FORM TWO NATIONAL ASSESSMENT (FTNA) 2015 RESULTS

FORM TWO NATIONAL ASSESSMENT (FTNA) 2015 RESULTS

Tusiime watia fora ufaulu kidato cha pili
ASILIMIA 99 ya wanafunzi wa shule ya sekondari Tusiime waliofanya mtihani wa kidato cha pili wamefaulu kwa daraja la juu yaani ufaulu uliojipambanua (Distinction).
Akizungumzia matokeo hayo ofisini kwake, Mkuu wa shule hiyo, Emil Rugambwa alishukuru kwa matokeo hayo mazuri na kusema kuwa mipango waliyonayo ni kuhakikisha wanaendelea kuwa juu kielimu.
Alisema jumla ya wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 318 na kati ya hao, 314 sawa na asilimia 99 wamepata ufaulu uliiojipambanua yaani Distinction hali ambayo imewapa faraja.
Rugambwa alisema ni wanafunzi watatu tu waliopata daraja la Merit na mmoja aliyepata daraja la Credit.
Matokeo hayo yanaonyesha kuwa wanafunzi wengi wamepata wastani wa ufaulu GPA ya 5 ambao ni ufaulu wa juu kabisa na wengine wamefaulu kwa GPA kuanzia 4.6, 4.5, 4.8, 4.9.
Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa shule za Tusiime, Albert Katagira aliwapongeza walimu wake kwa kazi na jitihada kubwa walizofanya kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kama hayo.
“Nawashukuru  wazazi, wanafunzi, wafanyakazi na wadau wa elimu kwa ujumla ambao wamewezesha kupata mafanikio haya  na natoa rai kwa serikali pamoja na wazazi kuendelea kushirikiana na uongozi wa shule za Tusiime katika kutoa elimu bora kwa vijana wetu,” alisema
“Napenda kuwahakikishia wazazi kwamba kutokana na mifumo na uongozi bora tulionao tusiime tutaendelea kutoa elimu bora na hakuna mzazi hata mmoja ambaye atajutia kumleta mtoto wake hapa Tusiime kwani tutahakikisha tunatimiza majukumu yetu katika kuwapa elimu vijana wetu kuhakikisha kila mtoto aliyeingia Tusiime anapata ufaulu wa juu,” alisema
Katagira alisema mipango ya shule hiyo ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayejiunga na shule hiyo anapata ufaulu uliojipambanua yaani GPA inayoanzia 4 na kuendelea katika mitihani ya kitaifa.
Akizungumzia siri ya ufaulu huo mzuri, mmoja wa wanafunzi waliopata GPA ya 5, Rahma Salum ambaye alipata alama A kwenye masomo 11  alisema nidhamu, kujituma kwa walimu, uongozi bora na ushirikiano wa karibu kati ya shule, wazazi na wanafunzi wenyewe ndio umewafikisha hapa.
Mwingine ambaye naye amepata GPA ya 5, Harson Mamkwe ambaye naye alipata alama A kwenye masomo 11 aliushukuru uongozi wa shule kwa kuwawekea mazingira rafiki katika kusoma na kuwasifu wanafunzi wenzake kwa ushirikiano katika masomo na kujituma kwao hivyo kupelekea ufaulu huo mzuri.
“Mazingira mazuri ya kujisomea yamechangia sana, mfumo wa malezi hapa shuleni na kujituma kwa walimu ambao wanatufundisha na kuwa karibu na sisi kila tunapowahitaji na hiyo imekuwa chachu kwa mafanikio haya,” alisema.
FTNA-2015